Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump, ametifua zogo jingine kwa kutoa matamshi yaliyotafsiriwa kuwa yanayowachochea wanaotetea haki za kumiliki bunduki kuchukua hatua zitakazomzuia Hillary Clinton.
![]() |
Akizungumza hapo jana katika mkutano wa hadhara, katika jimbo la North Carolina, Trump alisema Clinton akiachiwa kushinda, atawachagua majaji watakaopinga sheria ya haki ya kumiliki silaha nchini Marekani, matamshi ambayo yalionekana yanachochea kuangamizwa kwa mpinzani wake.
Maneno ya Trump ni hatari
![]() |
Hilary Clinton |
Mgombea urais wa Democrats Hillary Clinton
Punde baada ya matamshi hayo makali ya Trump, watu wengi katika mitandao
ya kijamii wamemshutumu mgombea huyo wa Republican kwa kutaka kuuawa
kwa Clinton.Idara ya usalama wa Marekani inayotoa huduma za usalama kwa Trump na Clinton ambayo ni nadra kuzungumzia masuala ya kisiasa imesema inafahamu kuhusu matamshi hayo yaliyotolewa na Trump, lakini haikusema kama itaanzisha uchunguzi.
Michael Hayden, mkurugenzi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani - CIA, amesema kiongozi ana wajibika sio tu kwa yale ayasemayo bali pia kwa yale watu wanayoyasikia.
Matamshi yenye utata kutoka kwa mgombea huyo wa urais wa chama cha Republican yanakuja hata baada ya maafisa 50 wa usalama wa Republican siku ya Jumatatu kuonya kuwa Trump atakuwa rais atakayeiendesha nchi hiyo kwa njia hatari katika historia ya Marekani iwapo atachaguliwa.
Kundi hilo la maafisa, ambao tayari wametangaza kwamba hawatampigia kura Trump, ni pamoja na wakuu wa masuala ya usalama wa ndani, wakurugenzi wa ujasusi, washauri waandamizi wa rais na mwakilishi wa zamani wa biashara nchini Marekani.
Hata hivyo, Trump hakuwasaza hata maafisa hao wa usalama wa Republican, akiwataja kuwa ni watu wa tabaka la juu waliofeli, wanaojaribu kung'ang'ania madaraka na wanaostahili kuwajibishwa kwa kuufanya ulimwengu kutokuwa salama.
Vigogo wa Republican wana mashaka
Vigogo wa Republican wenyewe wanakiri kuwa mgombea wao anaonekana kukosa tajriba ya kuiendesha Marekani, ana ufahamu mdogo wa katiba ya nchi, sheria, asasi, uelewa na ustahimilivu kuwahusu watu wa dini tofauti, uhuru wa vyombo vya habari na kuheshimu uhuru wa idara ya mahakama.
Wagombea urais Marekani Hillary Clinton na Donald Trump
![]() |
Hilary Clinton na Donald Trump |
Uchaguzi mkuu wa urais unatarajiwa mnamo tarehe 8 mwezi Novemba mwaka huu. Kura za maoni zinaashiria Clinton ana uungwaji mkono zaidi kuliko Trump miongoni mwa wapiga kura.
No comments:
Post a Comment